SHERIA

MAMBO YAKUFANYA UNAPOPOTEWA NA HATI NYUMBA/KIWANJA





NA  BASHIR  YAKUB - 
Hati miliki  ni  mali  inayohamishika  na  hivyo  inaweza kupotea.  Kupotea  kwa  hati miliki  kunaweza  kuwa  katika  mazingira  mengi.  Inaweza kupotea katika  mazingira ya  kuibiwa,  kufichwa  au  kutupwa  kwa  makusudi  kwa   malengo  mabaya  na  mazingira  mengine  yoyote  yanayofanana  na matukio  hayo.  Lakini   mara  kwa  mara  kupotea  kwa  hati  huhusishwa  na  mbinu  chafu  za  kubadilisha  umiliki   pasipo  uhalali  au  kutumika  katika  shughuli  za  kujipatia mikopo   pasi  na ridhaa  ya  mwenyewe. Makala  yataeleza   hatua  za haraka za  kuchukua iwapo  umetokewa  na jambo  kama  hilo.

1.HATUA  ZA  KUCHUKUA  HATI  INAPOPOTEA.

( a ) KUTOA  TAARIFA  POLISI  HARAKA
Hii  ni  hatua  muhimu  sana  na  ya  kwanza  kabisa  pale  tu hati  inapopotea.  Polisi  haipo  kwa  ajili  tu  ya kushughulikia  kesi  za  wizi  na  magomvi    bali  pia   kisheria  wamepewa  mamlaka  ya  kuandikisha  upotevu  wa  mali. Kituo  cha  polisi  ambacho  kinapaswa  kutumika   ni  kile  ambacho  nyumba/kiwanja  husika  kinapatikana.  Unapotoa  taarifa  polisi  hati  iliyopotea  huandikishwa   na  utapewa  namba  maalum  ya  kupotea. Taarifa  ya kupotea  huitwa  “lost report”.  

Umuhimu  wa  taarifa  hii ni  kuwa   ikiwa  hati  ile  imeibiwa  au  imechukuliwa  kwa  malengo  ambayo   si  halali  basi   itakapotumika  visivyo   wewe  utakuwa  umejitoa  katika   uhalifu  ule  na  hutowajibika  au  kutambua  matumizi  yale  yasiyo  halali.  

Usipotoa  taarifa  hii  ni  vigumu  kujitoa au  kutotambua  matumizi  iliyotumika  hati  yako   hata  kama  yalikuwa  ni  ya  kihalifu. Kwahiyo  hii  ni  hatua  ya  kwanza,   ya muhimu na  ya  haraka  kabla  ya  jambo  jingine.

( b ) Ikiwa  tayari umetoa  taarifa  polisi  na  una  wasiwasi  kuwa   kupotea  kwa  hati hiyo ni  mpango  ambao  pengine unalenga  matumizi  yasiyo  halali  basi  unaweza  kuweka  zuio. Zuio  huwekwa  mamlaka  za  ardhi   zilizokuwa  zimetoa    hati .  Zuio  huitwa “Caveat”.  Ni  hatua  ambapo  unaandaa  maombi  maalum  na  kuyapeleka  mamlaka   za  ardhi  kuomba  kuzuia  kufanyika  kwa  aina  yoyote  ya  mabadiliko  katika  umiliki  au  kuzuia  matumizi  yoyote ya  kukopea  hati  hiyo.

Maombi  ya  zuio yataambatana  na  picha  ndogo mbili , risiti  za malipo  ya  ushuru, kodi  na  tozo  za  ardhi.  Lakini  kubwa  ni  kuwa  ni  lazima  katika  maombi  hayo ueleze  sababu  ya  kwanini unaweka  zuio. Katika  hilo  sababu itakuwa  ni  kupotea  kwa  hati  katika  mazingira  yasiyoeleweka.  Ili  kulithibitisha  hilo   kuambatanisha  taarifa  ya  polisi  ya  kupotea ( lost  report) ni  lazima.   Maombi  haya  hulipiwa ada  maalum.

 2. IKIWA  HATI  IMEPOTEA  NA  UNAHITAJI  KUPATA  NYINGINE HATUA  NI  HIZI.

( a ) Andaa  maombi  maalum  ya  kuomba  kupatiwa  hati.  Maombi  hayo hufanana  na  yale  ambayo  ulikuwa  umeombea  hati  ya  awali  iliyopotea. Tofauti  hapa  ni  kuwa  katika  maombi  mapya   utaeleza  kuwa  unaomba  hati  nyingine  baada  ya  ile ya awali  kupotea.

( b ) Andaa  picha  ndogo  mbili  yaani  passport size  ambazo  zitatumika  kukaa  kwenye  nyaraka  mpya  za  maombi.

( c ) Ripoti  ya  polisi  ya  kupotea (lost  report)  ni  taarifa  muhimu  ambayo  ni  lazima  iwe  imeambatanishwa   katika  maombi  mpya. Hii  itaeleza  mazingira  yote  ya  kupotea    kwa  hati na  itakuwa  ni  taarifa  maalum  kuwa  hati  hiyo  haipo tena.

( d )  Kiapo  cha  mmiliki  kikieleza  na  kuthibitisha  kupotea  kwa  hati  huwa  kinahitajika.  Hata  hivyo  si  wakati wote  kiapo   hiki  huhitajika. Kwa  maana hiyo  kiapo  utajiandaa  nacho  tu  kama  dharula ambapo  ukitakiwa  kukiwasilisha  utafanya  hivyo  na  kisipohitajika  basi  haitakuwa  na  haja.

( d )  Lazima  uwe  na  nyaraka  nyingine  zinazohusu  umiliki  kwa  mfano  mkataba  wa  kununulia,   fomu  namba  29, 30, 35  na  nyaraka  nyingine  yoyote  ambayo  inaonesha  kuwa  wewe  ndio  ulikuwa  unahusika  na  umiliki  wa  eneo  hilo.

( d ) Mwisho  risiti  za  malipo  ya  kodi,  ushuru  na  tozo  za  ardhi   ziambatanishwe. Hizi  pia pamoja  na  mambo  mengine  husaidia  kuonesha  kuwa  ulikuwa  mmiliki  wa  hati  iliyopotea.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241 





UNATAKA KUFANYA TRANSFER (KUBADILI JINA) LA KIWANJA/NYUMBA,UTARATIBU WA HARAKA NI HUU.






Na Bashir Yakub.0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com

 Watu wengi wamenunua viwanja/nyumba lakini mali hizo zimeendelea kubaki katika majina ya waliowauzia. Wapo ambao imepita hata miaka kumi tangu wanunue maeneo lakini bado hawajabadili jina kuingia jina lake. Zipo sababu nyingi zinazosababisha hali hiyo lakini moja ni watu kutokujua umuhimu wa kubadili jina kwa haraka. Hapa sizungumzii tu kubadili jina isipokuwa nazungumzia kubadili jina kwa haraka. Kupitia makala haya napenda kuwaamsha watu kuhusu umuhimu mkubwa wa kubadili jina kwa haraka iwapo umenunua nyumba/kiwanja kwa mtu. Ni muhimu sana kufanya hivyo na itakuepusha na mambo mengi.

1.KAMA HUJABADILI JINA ALIYEKUUZIA BADO NDIYE MMILIKI.

Ikiwa kutatokea mgogoro wa umiliki wakati ambao umenunua nyumba/kiwanja na hujabadili jina kwenda kwenye jina lako kuna hatari kubwa zaidi ya kupoteza ulichonunua. Hii ni kutokana na ukweli kuwa utapokuwa unatatuliwa mgogoro wa nani mmiliki swali la kwanza huwa ni nani ambaye nyaraka ya umiliki ina jina lake. Yule ambaye jina lake linaonekana kwenye hati au leseni ya makazi ndiye hupewa kipaumbele na kwa mujibu wa sheria mwenye jina kwenye hati au leseni ya makazi ndiye mmiliki. Wewe uliyenunua utakuwa na mkataba na jina lako litakuwa kwenye mkataba lakini pamoja na kuwa na jina kwenye mkataba bado huwezi kulinganisha mkataba na hati au leseni ya makazi. Jina linalotokea kwenye hati au leseni ya makazi huwa na nguvu zaidi kuliko lile la kwenye mkataba

2.UMUHIMU WA KUBADILISHA JINA KWA HARAKA.

Upo umuhimu mkubwa mara tu baada ya manunuzi ya kiwanja/nyumba kukimbilia hatua za kubadili jina. Ni vyema wakati unajipanga kununua nyumba/kiwanja ukajipanga moja kwa moja na hatua za kuanza kubadili jina mara baada ya kukamilika kwa mkataba wa manunuzi. Mara nyingi tumekuwa tukiwashauri watu kuwa mkataba wa manunuzi unapokuwa umekamilika leo basi hakikisha kesho unaanza taratibu za kubadili jina( transfer). Ni utaratibu huu pekee utakaokufanya kujiamini na ulichonunua. Pia unapotokea mgogoro kabla ya kubadili jina kuanzia hapo unakuwa na nafasi ndogo ya kuweza kubadili jina kwakuwa kama mgogoro utaenda mahakamani inaweza kutokea kuzuiwa kufanya hivyo mpaka kesi itakapokwisha. Kesi yenyewe itaisha lini haijulikani . Kama ikiisha baada ya miaka kumi, kumi na tano ina maana muda wote huo utakuwa una mali ambayo ni kama si ya kwako.

3.UTARATIBU WA KUBADILI JINA( TRANSFER) BILA USUMBUFU

( a ) Kwanza hakikisha una mkataba wako wa kununulia ambao una muhuri wa wakili uliondaliwa kitaalam huku ukiwa na picha za wote mnunuzi na muuzaji ikiwa ni pamoja na sahihi zenu wote. Kwa ufupi hakikisha mkataba wako ni mzuri ambao una viwango vya kisheria ili kuepuka kurudishwa rudishwa kwa ajili ya marekebisho au kukataliwa kabisa uwapo mamlaka za ardhi. 

( b ) Pili hakikisha una fomu namba 29 ambayo ni taarifa ya kutoa umiliki .Fomu hii ni taarifa maalum ambayo aliyekuuzia anatoa taarifa kwa kamishna wa ardhi kuwa anataka kutoa umiliki wake kwa wewe mnunuzi. Atakuwa akizungumza kwa mtindo wa kiapo kuwa mimi fulani wa sehemu fulani ninatarajia kutoa umiliki wangu wa ardhi wa eneo fulani kwa fulani fulani. Mwisho muuzaji ataweka sahihi yake na atakuwa ameichambua plot anayotoa umiliki na anuani zake za makazi zitakuwa zimeoneshwa vyema. Fomu hii hupatikana mamlaka za ardhi na kwenye ofisi za wanasheria. 

( c ) Tatu ni kujaza fomu Namba 30 ambayo ni kudhibitisha nia ya kutoa umiliki. Ile ya juu namba 29 inatoa umiliki wakati hii inathibitisha nia ya kutoa au kuachia umiliki kwenda kwa mnunuzi. Hivyo hii namba 30 ni msisitizo wa namba 29. Hii ni kutokana unyeti wa masuala ya ardhi. Aidha taarifa nyingine katika fomu hii ni zilezile zilizo katika fomu namba 29. Fomu hii nayo hujazwa na muuzaji tu na hupatikana mamlaka za ardhi au ofisi za wanasheria.

( d )Nne baada ya fomu hizo hapo juu sasa inakuja fomu namba 35 ambayo ni fomu rasmi ya kuhamisha umiliki ( transfer of right of occupancy). Katika fomu hii ndimo muuzaji anapotamka rasmi kuachia umiliki na kuutoa kwa mnunuzi ikiwa ni pamoja na kuainisha bei ya mauzo. Fomu hii itachambua nyumba/kiwanja ambacho kimetolewa umiliki na hii itakuwa na majina yote mawili yaani muuzaji na mnunuzi. Pia itakuwa na sahihi zao wote ikiwa ni pamoja na picha. Pia itakuwa na muhuri wa wakili akiwa kama shahidi wa wote wawili muuzaji na mnunuzi. Fomu hii nayo hupatikana mamlaka za ardhi na ofisi za wanasheria.

4.LAZIMA UWE NA RISITI ZA KODI

Hiki ni kiambatanisho kingine kinachohitajika. Utatakiwa kupeleka taarifa ya uthamini wa ardhi mamlaka ya mapato ambapo kupitia taarifa hiyo watakupa hesabu za kodi utalipa na utapewa risiti na risiti hiyo ndiyo utakayoambatanisha kwenye maombi yako. 

5.USHAURI WA KITAALAM.
 Hakikisha siku ya kununua nyumba/kiwanja inakuwa ndio siku ya kuanza hatua za kufanya transfer. Kuchelewa kunapunguza hadhi yako ya umiliki na kunakuweka karibu zaidi na mgogoro. Ni vigumu kumaliza mgogoro kwa usalama pindi utakapotokea ukiwa haujafanya transfer. Zingatia sana haya.

1 comments: