Lakini mwanamke huyu hivi sasa yu mashakani, kwani ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi umeshika kasi nchini, hivyo hutesa na hatimaye kuua maelfu ya wanawake.Saratani ni mfumo au tabia ya chembe hai nyeupe kukua katika sehemu ya mwili wa binadamu katika mfumo usio wa kawaida.
Hivyo basi, chembe hizo zikikua katika shingo ya kizazi cha mwanamke, kinyume cha taratibu, hiyo huitwa saratani ya shingo ya kizazi.
Dk Henry Mwakyoma, Daktari Bingwa wa Kitengo cha Patholojia katika hospitali ya Muhimbili, amefanya utafiti kati ya Februari 2001 na Februari 2002. Lengo la utafiti huo lilikuwa ni kuangalia ukubwa wa tatizo la saratani ya shingo ya kizazi kwa hapa nchini.
Aliwapima wanawake 224 kutoka mikoa mbalimbali nchini waliopewa rufaa ya kufika Muhimbili. Katika wagonjwa hao, 193, sawa na asilimia 86.2 waligundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi na 31 sawa na asilimia 13.8 walikuwa hawana saratani.
Dk Mwakyoma anasema, miongoni mwa waliokutwa na saratani hiyo, walikuwa na umri wa kuanzia miaka 24 hadi 82.
"Katika hao walioathirika zaidi walikuwa ni wenye umri wa miaka 40 hadi 49 na wengine walikuwa na umri wa chini ya miaka 40," anasema Mwakyoma.
Daktari bingwa huyu alifanya utafiti mwingine kuhusu saratani ya aina hii kati ya mwaka 1980 hadi 1984 katika nchi za Tanzania na Uswisi. Lengo lilikuwa kuangalia ukubwa wa tatizo hili katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea.
Utafiti ulifanyika katika hospitali kuu za rufaa Tanzania, ambazo ni Bugando, KCMC, hospitali ya rufaa ya Mbeya na Muhimbili.
"Niliamua kufanya utafiti huo katika hospitali za rufaa nchini ili kupata namba ya wagonjwa katika mikoa mikubwa," anasema Dk Mwakyoma.
Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa, katika hospitali ya KCMC asilimia 13.9 ya wanawake waliopimwa waligundulika na saratani ya shingo ya kizazi. Bugando, asilimia 20, Mbeya asilimia 24.3, na Muhimbili walikuwa ni asilimia 18.4 ya wanawake.
"Katika aina kumi za saratani duniani, basi saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuwaathiri wanawake hapa nchini," anasema Dk Mwakyoma.
Chanzo cha saratani hii
Dk Mwakyoma anabainisha kuwa, sababu kubwa ambayo hupelekea wanawake wengi kupata saratani ya shingo ya kizazi ni matokeo ya ufanyaji wa ngono.
"Kufanya ngono ninaweza kusema ni sababu kubwa na sababu nyinginezo huambatana na hizo lakini kichocheo kikubwa ni ngono," anasema.
Anasema, sababu nyingine zinazosababisha mwanamke kupata saratani hii ni kufanya mapenzi katika umri mdogo. Wanawake wengi wanaofanya mapenzi chini ya miaka 16, wapo katika hatari kubwa.
"Katika wanawake waliogundulika na saratani, asilimia 14.95 kwa wastani walikuwa wameanza kufanya mapenzi wakiwa na umri wa miaka 14 hadi 25," anafafanua Dk Mwakyoma.
Asilimia 17.8 ya wanawake hao, walikuwa wameolewa wakiwa na umri wa kuanzia miaka 11 hadi 35.
Hali kadhalika kati ya wanawake 161, 71 (44%) ya waliopimwa na kugundulika na saratani ya shingo ya kizazi, waliolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18.
Sababu nyingine inayosababisha saratani ya shingo ya kizazi ni mimba na kuzaa. Dk Mwakyoma anasema, idadi ya ujauzito kwa wanawake husababisha saratani ya shingo ya kizazi.
Kwa mfano, mtu ambaye amebeba ujauzito zaidi ya mara sita (kwa hapa nchini) yupo katika hatari ya kupata saratani ya aina hii.
"Katika wanawake 193 niliowapima, 136 waliwahi kupata mimba zaidi ya mara nne, nasisitiza si kuzaa, yaani wastani wa mimba ulikuwa ni saba," anasema.Katika kiwango cha kimataifa, wastani wa kubeba mimba usio katika hatari ya kusababisha saratani ya shingo ya kizazi ni mara nne.
"Sababu nyingine ni kiwango cha kuzaa, wanawake wanaozaa sana huwa katika hatari, kwa mfano katika wanawake 193 niliowafanyia utafiti, 107 walikuwa na watoto zaidi ya wanne," anasema.
Anasema, idadi ya wapenzi ni sababu nyingine. Mwanamke mwenye wapenzi wengi, bila shaka atakuwa anafanya mapenzi kwa kiwango kikubwa, hivyo basi kupata magonjwa ya zinaa yanayosababisha saratani hii ni rahisi.
Vilevile wanawake walioolewa mara nyingi nao wamekuwa wakigundulika na saratani ya shingo ya kizazi. Kwa mfano, wenye historia ya kupewa talaka kisha kuolewa tena, au wajane wanaoolewa kwa mara nyingine na wanaotengana na wapenzi katika vipindi tofauti tofauti.
"Wapo wanaume hatari ambao nao huchangia wanawake kupata saratani ya shingo ya kizazi, hawa kitaalamu tunawaita High Risk Male Sexual Partner' hawa wanapokuwa na wapenzi wengi hutokea wakawaambukiza wanawake magonjwa ya zinaa."
Dk Mwakyoma anaongeza kuwa, ugonjwa wa zinaa ambao ndicho kichocheo kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi ni Human Papiloma Virus 16 na 18 (HPV).Ugonjwa huu unapokomaa huzalisha seli ambazo hukua kinyume na utaratibu na kuanza kushambulia sehemu ya shingo ya kizazi.
Jambo lingine linalosababisha saratani ya shingo ya uzazi ni usafi katika sehemu za siri za mwanamke. Wanawake wanaofanya usafi sehemu zao za siri kwa kutumia bidhaa au baadhi ya vifaa visivyofaa kutumiwa ukeni huweza kupata saratani hii. Kwa mfano, bidhaa zenye kemikali ya coal tar,' ambayo mara nyingine huwekwa kwenye sabuni ama manukato.
Dalili
Dk Mwakyoma anasema, ni vyema na muhimu mno kwa wanawake kupima afya zao za uzazi kabla ya kuona dalili.
Mwanamke anapoona dalili basi saratani huwa imefikia hatua mbaya ya kifo. Anasema hatua hizi zipo katika makundi ambayo yamegawanyika.
"Ipo hatua ya mwanzo (pre-invasive) ambapo saratani bado haijafanya mashambulizi katika mwili kwa asilimia kubwa na hatua ya pili (invasive) ambayo imegawanyika katika hatua nne na hatua hii saratani huwa imeshasambaa katika sehemu nyingine za mwili," anasema.
Anazitaja dalili kuu za ugonjwa huu kuwa ni kutokwa na damu kwa wingi hasa wakati wa hedhi. Nyingine ni kutoa maji maji yenye harufu mbaya ukeni, na kupata maumivu sambamba na kutoka damu baada ya kufanya tendo la ndoa.
Dk Mwakyoma anatoa ushauri kwa serikali kuwa, itungwe sera ambapo ni lazima kila mwanamke aliye katika umri wa kufanya mapenzi akapimwe saratani ya shingo ya kizazi.
"Ili kupunguza tatizo ni bora kuwapima, tunatumia kipimo cha pap-smear' ambacho hata Uswisi hutumia kuwapima wanawake," anasisitiza
Naye Dk Innocent Mosha, wa kitengo cha patholojia Muhimbili anasema, ni vyema wasichana wadogo wafuate maadili na wajiepushe na vitendo vya ngono katika umri mdogo ili kujiepusha na maradhi haya.
Takwimu za mwaka 2010 kutoka Shirika la Afya Duniani, (WHO) zinasema, kwa Tanzania wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka na 4355 kati yao hupoteza maisha.
0 comments:
Post a Comment